Roho ya kukataliwa inawasumbua watu wengi. Wengi wanaosumbuka na kukataliwa inawezekana walikuwa na wazazi wasiojali, wazazi walitengana, wamelelewa na mzazi wa kambo, hawakuwa vizuri darasani, n.k. Kukataliwa kunaumiza sana na kunaua kabisa hali ya kujiamini na shetani huitumia sana kuharibu maisha ya watu. Shetani anawafanya watu wasahau kabisa juu ya upendo wa Mungu na kuendelea kuumia na kuteseka.
EFE. 3:19
"na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu."
Kukataliwa kunaleta vidonda kwenye hisia na visipotibiwa hukua na kuwa vidonda vya kiroho kama kutokusamehe, wivu, chuki, uchungu na kumlaumu Mungu. Vidonda hivi hufungua milango kwa roho chafu kukuingilia kupitia milango hiyo. Shetani anafurahia moyo wako ukijaa mawazo mabaya juu ya watu wengine unaowaona kwamba hawajakutendea mema.
Kukataliwa kunamfanya mtu kuwa na tabia zifuatazo:
1. Uasi
2. Unafiki (ukiwa mbele za watu fulani unabadilika ili ukubalike)
3. Kukataa wengine
4. Kila wakati kujihisi kuwa unakataliwa
5. Kuhitaji sana kukubaliwa na kila mtu
6. Kujihurumia
7. Kutokuwa tayari kukosolewa au kusahihishwa
8. Kutokuweza kupokea wala kuonyesha upendo.
9. Kumlaumu Mungu kwa hali uliyonayo
10. Kiburi
11. Ukiwa hata ukizungukwa na watu.
12. Kujiona huna thamani, wala tumaini
13. Wivu, chuki na husuda.
Wengine wanahisi kukataliwa wakati si kweli. Roho hii ya kukataliwa inakufanya uone kama kila ambaye hajafanya jambo fulani kukusaidia au kukufurahia basi anakukataa. Biblia inasema aonavyo nafsini mwake ndivyo alivyo. Pia kuna wanaojikataa wenyewe na kupelekea kujichukia. Hali hii hutokana na kushindwa kujisamee kwa kosa fulani ukilotenda siku za nyuma na likakuletea madhara makubwa.
Tutaendelea sehemu ya pili jinsi ya kukabiliana na hali hii.
Source: Woman of Christ
0 comments:
Post a Comment