Monday, July 29, 2013

WANAWAKE WENYE TAMAA YA PESA NA MALI NI "MAJANGA"..!! nimeitoa sehemu

Mama yangu mzazi amekuwa mwalimu na kiongozi wangu mkubwa katika masuala ya kibiashara na kifamilia. Kabla sijachumbia amewahi kunipa somo la tahadhari (kwa lugha ya kikinga); kuhusu wanawake wenye tamaa; alisema, “Mwanangu Albert uwe makini sana na mabinti wenye tamaa ya mali na fedha. Mabinti wa namna hii hawafai sio tu kuwaoa lakini usithubutu hata kutengeneza urafiki nao; watakumaliza! Mwanamke mwenye tamaa huwa hashibi kwa sababu tamaa ni pepo linalolilia kila kizuri kinachotokea na lisiloshiba kwa lolote linalofanyiwa. Hata ukimnunulia magari yote mazuri duniani, ukamjengea na majumba mazuri, ukamnunulia na ndege bado mwanamke mwenye tamaa hawezi kuridhika na wewe. Vile vile wanawake wenye tamaa hawana shukrani kwa wanayofanyiwa kwa sababu huamini kuwa ni haki yao” Mwishoni mama akamalizia kwa kuniasa hivi; “Fanya biashara zote halali duniani lakini usijiingize kwenye biashara ya kununua ama kulipia mapenzi. Waache wapumbavu waambatane na wanawake wenye tamaa na wenye kulipisha mapenzi; lakini wewe mlilie Mungu akupatie mke mwema”