Thursday, November 1, 2012

Sifa za Mume Mwema

Shalom,

1. Awe mwenye kumcha Mungu

Mume mwema ni yule anayeheshimu nafasi ya Mungu katika maisha yake, anayemcha Mungu na kuepukana na uovu wa kila aina. Anatambua kwamba Mungu ndiye anayepaswa kuongoza maisha yake na si vinginevyo.
Kumbukumbu 6:5 Nawe mpende BWANA Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.

2. Mwenye kumpenda mke wake kama nafsi yake

 
Kumpenda mke wake zaidi ya kitu chochote iwe ni wazazi, kazi, biashara, watoto n.k. Mume mwema siku zote huthamini nafasi ya mke katika maisha yake na mara zote mke wake ni namba moja kwake.
Mwanzo 2:24 Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.

Efeso 5: 25,28 Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda kanisa, akajitoa kwa ajili yake,..vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe.

 
3. Mwenye uwezo wa kuiongoza familia yake

 
Inashangaza kuona baadhi ya waume hawawezi kusimama kama viongozi katika nyumba zao. Wanasahau kama Mungu kawaweka kama viongozi wa familia na mke ni msaidizi wake. Utakuta wengine wanaaacha jukumu hilo kwa mkewe kwa kupenda au kwa kutokupenda na wengine wanajikuta wamewafanya wazazi wao au ndugu zao wengine kusimama kama viongozi wa familia.Biblia inaweka wazi kuwa mume ni kichwa cha ndoa, ni lazima kila mume atambue hilo na ahakikishe anasimama kwenye nafasi yake kwa uaminifu bila kujali hali yake, wadhifa, kipato, huduma au chochote kile.

Efeso 5:23 Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe; kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili.

4. Mwenye Kuihudumia Familia Yake

 
Mume mwema lazima ahakikishe anafanya kazi na kuipatia familia yake mahitaji ya kila siku. Haijalishi mkewe anafanya kazi au la, yeye kama mume anajukumu la kuihudumia familia yake na hii ni sehemu ya uongozi wake. Hapa pia inajumuisha na kuilinda familia yake juu ya hatari zote na kuhakikisha wana furaha na amani ya kudumu. Ili mke na watoto waweze kuwa na amani ni lazima wahakikishiwe usalama wao kimwili, kiroho na kiuchumi.
1Timotheo 5:8 Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini.

 
5. Mwenye kuwafundisha watoto njia inayopasa

 
Mume kama kiongozi wa familia anajukumu la kuwafundisha watoto njia inayofaa akisaidiana na mke wake. Waume wengi wanafikiri kazi ya kuwafundisha watoto ni ya mama wao ni kutoa tu adhabu pale wanapoona mtoto amekosea lakini hawajishughulishi katika kuwafundisha. Mume mwema lazima alitambue jukumu lake la kuwafundisha watoto neno la Mungu na misingi ya maisha ya mkristo.

 
Kumbu kumbu 6: 6-7 Na maneno haya ninayokuamuru leo,yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena, uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.

 
Efeso 6:4 Nanyi wakina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya BWANA.

 
6. Mwenye kumheshimu mke wake

 
Imezoeleka kuwa mke ndiye anayepaswa kimheshimu mume, lakini biblia inawataka pia waume kuwahepa heshima wake zao na kuishi nao kwa akili. Haipaswi mume kufanya maamuzi yoyote yanayohusu familia bila kumshirikisha mke wake, yawe madogo kama lini mgeni fulani aje hadi makubwa kama ujenzi au kuanzisha biashara. Mke ni sehemu ya mume hivyo ni lazima mume ampe heshima yake na kuthamini mawazo yake na mchango wake hata kama mke hafanyi kazi ya kuingiza kipato. Kumbuka mke anabeba jina la mume wake na ni sehemu ya mume wake, inahuzunisha kuona waume wengine wakiwadharau wake zao mbele ya ndugu zao au marafiki. Haipasi kabisa kumgombeza au kumsema vibaya mke wako mbele za watu, iwe ni ndugu, watoto au mwingine yeyote.

1Petro 3:7 Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe.

Source:Women of Christ

Reactions:

1 comments:

  1. I WISH WANAUME WOTE WANGEYAFANYA HAYA.
    NYUMBA ZINGEDUMU. UTAKUWA MVUMILIVU LAKINI BINADAMU SI KISIKI WALA MAJI, UNACHOKA NA KUTAFUTA AFUENI.

    ReplyDelete