Wednesday, September 11, 2013

MKE MWEMA...

Kitabu cha mithali 31 kuanzia msitari wa 10 hadi 31 kimeelezea sifa mbalimbali za mke mwema, tuangalie kwa uchache sifa hizo kwa kuzichambua katika maeneo tofauti.
1. Imani
Mithali 31:26, 29, 30
Mke mwema anayashika na kuyafanyia kazi maneno ya Mungu na ni mtu ambaye anamtumikia Mungu kwa moyo wake wote na akili yake yote. Anatafuta makusudi ya Mungu katika maisha yake na kuyafuata. Zaburi 119;15

2. Ndoa
Mithali 31:11-12, 23, 28
Mke mwema humuheshimu mume wake na anahakikisha anamtendea mambo mema siku zote za maisha yake. Ni wa kuaminika na msaidizi kwa mume wake. Efeso 5:22-24, 1Petro 3
3. Malezi
Mithali 31: 26, 28
Mke mwema anawafundisha watoto wake njia za Mungu na pia anawatunza kwa upendo. Huwafundisha kwa hekima na kuwaelekeza njia iwapasayo kuiendea. Mithali 22:6
4. Huduma
Mithali 31:12-15, 17, 20
Mke mwema anamhudumia mume wake na familia yake yote kwa ukarimu na upendo. Anahakikisha wanapata chakula kilicho bora na chenye afya. Ni mtu mwenye huruma na ukarimu.
5. Mali
Mithali 31:14, 16, 18
Mke mwema anatafuta kwanza ushauri wa mumewe kabla ya kutumia fedha na pia anafanya manunuzi kwa hekima. Ni muangalifu kununua bidhaa zenye ubora kulingana na mahitaji ya familia yake.Efeso 5:23
6. Nyumba
Mithali 31:15, 20-22, 27
Mke mwema ni mtu anayeifanya nyumba iwe mahali pa kuishi. Anatengeneza mazingira ya kuvutia kwa familia yake na wageni wote na anawahudumia watu wake wote kwa ukarimu. 1pet 4:9, Ebrania 13:2
7. Muda
Mithali 31:13, 19, 27
Hutumia muda wake vizuri na kuhakikisha anakamilisha kazi zake za kila siku. Kamwe hapotezi muda katika kufanya mambo ambayo hayampendezi Mungu na yasiyo na faida.
8. Uzuri / Urembo
Mithali 31:10, 21-22, 24
Ni mrembo na mwenye thamani, ana uzuri wa ndani unatoka kwa Yesu Kristo. Anatumia ubunifu wake na utanashati wake kuleta uzuri katika maisha yake na ya watu wake.
Mungu atusaidie ili maisha yetu yaonyeshe kweli tunamjua na kumwamini yeye.
Ubarikiwe na Bwana Yesu!

Reactions:

0 comments:

Post a Comment