Friday, July 12, 2013

Sikia Hii...

 LEO tutazungumzia tatizo la kulegea kwa misuli ya sehemu za siri za mwanamke au kitaalamu Vaginal prolapsed.
Tatizo hili huwatokea zaidi wanawake wenye umri mkubwa ingawa pia linaweza kuwakumba hata wenye umri mdogo. Tunapozungumzia kulegea kwa misuli ya sehemu za siri hapa kuna tofauti kidogo na kutanuka kwa misuli hiyo.
Tukizungumzia kulegea ina maana misuli ya ukeni inashindwa kubana na kuachia njia. Hapa misuli inayoachia njia inapolegea hata ukichuchumaa huhisi nyama zimejaa ukeni.
Kulegea kwa misuli hiyo hutokana na matatizo mbalimbali na hasa mwanamke anapozaa uzazi wa karibukaribu, au kutokana na matatizo ya vichocheo (Hormones) za kike, pia kunaweza kusababishwa na magonjwa sugu kama kansa, kifua kikuu (TB)  na maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi na magonjwa  mengine ya zinaa.
Mama anaweza kupatwa na tatizo hili anapojifungua kwa kuongezwa njia.Tatizo hili la kulegea misuli pia huchangiwa na umri mkubwa kwa hiyo kwa wanawake wazee hasa wanapofikisha umri wa miaka 70 na kuendelea wanaweza kupatwa na tatizo hili.

Dalili 
Mwanamke mwenye tatizo hili wakati wa kujisafisha ukeni atahisi kama sehemu yake ya siri  imeziba au imejaa nyama na inamfanya atumie muda mrefu kujisafisha. Mara kwa mara atakuwa anasumbuliwa na kuwashwa sehemu hiyo na kutokwa na uchafu wakati wa kufanya tendo la ndoa.
Pia atahisi maumivu wakati wa kufanya tendo la ndoa. Baada ya muda maumivu yanakuwa makubwa mpaka inafikia mwanamke huumwa tumbo chini ya kitovu mara kwa mara.
Dalili nyingine ni mwenendo wa siku za hedhi huvurugika na inakuwa shida kupata ujauzito. 
Hali ya kulegea kwa misuli ya uke pia humuathiri hata mume kwani naye hushindwa kufurahia tendo la ndoa.
Kulegea au kutanuka kwa uke huathiri uhusiano wa kindoa kwani mama hafurahii tendo hilo kutokana na kupata maumivu badala ya kustarehe.
Mwanamke mwenye tatizo la kutanuka kwa sehemu zake za siri anaweza kujigundua mwenyewe hata kabla ya kumuona daktari kwani dalili tumezitaja hapo juu .

TIBA NA USHAURI
Muone daktari wa magonjwa ya akina mama kwa uchunguzi na ushauri wa tiba.
Vipimo mbalimbali vitafanyika kubainisha tatizo kama vile kipimo cha damu, vipimo vya ukeni mfano kama vile kiitwacho Speculum examination, kuotesha uchafu wa sehemu za siri na kuvipima na kama mama ana maumivu ya tumbo vipimo ataweza kupimwa kwa Ultrasound.
Daktari anaweza kuangalia mwenendo wa mfumo wa homoni na historia ya tatizo kwa ujumla kwa mama mhusika na akafanya tathmini kwani itasaidia kujua kama tatizo ni la kuzaliwa nalo, uzazi wa karibukaribu au ni nini. Uchunguzi huu utafanyika ili kuweza kumpatia mgonjwa tiba.
Tiba ya maradhi haya hutolewa katika hospitali kubwa au katika kliniki maalum za magonjwa ya wanawake ambapo mwenye tatizo hupewa dawa za kurekebisha misuli hiyo au hufanywa kwa njia ya upasuaji mdogo ili kumrudisha mwanamke katika hali yake ya kawaida.

Source:Global Publishers