Tanga, Tanzania. Bibi harusi, mkazi wa Chanika mjini Handeni, Mkoa wa Tanga, Levina Mmasi (23) amefariki dunia saa moja kabla ya ndoa kufungwa kanisani na kuilazimu kamati ya harusi kushughulikia shughuli za msiba.
Mwanamke huyo alifariki Jumamosi iliyopita na msimba huo umekuwa gumzo kubwa mjini Tanga huku wananchi wakisema kuwa ni tukio ambalo halijawahi kutokea.
Msemaji wa familia, Firmin Mrimasha amesema chanzo cha kifo cha Levina ambaye alikuwa mjamzito alijifungua siku moja kabla ya ndoa na ilibainika kwamba alikuwa na malaria baada ya kupelekwa Hospitali ya Wilaya ya Handeni.
Baada ya vipimo vya daktari, mwanamke huyo alikutwa na malaria na kulazwa kwenye hospitali hiyo kwa matibu.
"Huyu bibi harusi alijifungua Alhamisi mtoto wa kiume baada ya kubeba ujauzito wa miezi saba, lakini ghafla Alhamisi alipata homa tukampeleka hospitali ambako alilazwa, akakaa Ijumaa na Jumamosi saa 8.05 alikafariki dunia wakati akisubiriwa kwenda kanisani kufunga ndoa ambayo ilikuwa ifanyike saa 9.00 alasiri siku hiyo.
“Inasikitisha sana ila imeshatokea yaani marehemu amefariki siku moja kabla ya ndoa yake, ndoa ilikuwa ifungwe saa 9:00 naye akafariki saa 8:00 na mtoto wake naye alifariki muda mfupi baada ya mama yake kufa,"amesema Mrimasha.
Akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa kamati ya harusi hiyo Abdi Kipacha amesema tukio hilo ni la kwanza kwake tangu kuzaliwa na kamwe hawezi kulisahau.
Amesema kamati zote zilishamaliza maandalizi ya harusi ila ghafla wakapewa taarifa kwamba bibi harusi amefariki dunia.
“Nilipanga kamati zangu zote na kuzipa majukumu yao, tulichokuwa tukisubiri kuambiwa kama bibi harusi ataweza kuja, lakini ghafla tukapewa taarifa kwamba amefariki dunia, ilikuwa ni vigumu kuamini, lakini ni kweli imetokea na inasikitisha kwani si jambo la kawaida,”amesema Kipacha.
Marehemu alikuwa Mwalimu wa Shule ya msingi mkoani Lindi. Mwili wa bibi harusi huyo ulisafirishwa jana kupelekwa Machame mkoani Kilimanjaro kwa mazishi ambayo yatafanyika leo Jumatato.