Imezoeleka kuwa mtu akisikia kuhusu mithali 31 basi moja kwa moja anajua kuwa ujumbe huo unawahusu wanawake. Ni kweli kuwa mistari hii ni mahususi kwa ajili ya wanawake, ila pia ni ukweli usiopingika kuwa mwanamke anayezungumziwa hapa ana mume. Biblia haijatoa sifa za mchumba mwema bali mke mwema, na huyu mke mwema ameweza kuwa mwema sababu mumewe pia ni mume mwema. Kwa haraka sifa za mke mwema zilizopo hapa ni mchapakazi, mkarimu, mjasiriamali, anayejali, mtunzaji wa familia yake.
Mume wa mke huyu amezungumziwa pia kwa mema: 1. Mstari wa 11 “Moyo wa mumewe humwamini, Wala hatakosa kupata mapato”Anamwamini mke wake. Sio kumtawala kwa mabavu wala kumhisihisi vibaya. Aliamini kuwa mke wake anamuwazia mema na nia yake ni kujenga familia bora na imara na sio kushindana naye.
Alipomuamini mke wake, alimpa nafasi ya kuonyesha uwezo wake na hivyo familia kunufaika. Mwanamke aliyeolewa anahitaji kujiona anaaminiwa na mume wake ili aweze kukitoa kwa nguvu na uwezo wote katika kujenga familia imara.
2. Mstari wa 23 “Mume wake hujulikana malangoni; Aketipo pamoja na wazee wa nchi.”Ni mtu anayejishughulisha na masuala muhimu ya maendeleo ya jamii yake. Hafuati tu mambo yake mwenyewe bali pia maslahi ya jamii yake kwa kuketi pamoja na wazee wa nchi. Ni mtu anayeshirikiana na wengine3.Mstari wa 28,29 “Wanawe huondoka na kumwita heri; Mumewe naye humsifu na kusema, Binti za watu wengi wamefanya mema, Lakini wewe umewapita wote.”
Anamsifia mke wake kwa yale anayoyatenda kwake na kwa familia nzima. Haoni aibu kumsifia mkewe. Mume huyu alionyesha kujali ma kuthamini mchango wa mke wake katika familia na akamsifia kwa hilo.
Ni muhimu kila mume akaiga mfano wa mume huyu: - Anamwamini mke wake. - Anajishughulisha na jamii yake, hajitengi na watu anaoishi kati yake. - Anamsifia na kumthamini mke wake.
Source: Women of Christ
0 comments:
Post a Comment