Tuesday, October 30, 2012

Mume amlipuwa mke kisa wivu wa mapenzi.. Makubwa haya kumbe mke anauma???

MWANAMKE aliyefahamika kwa jina la Subira Malefya (53), mkazi wa Kijiji cha Ipinda wilayani Kyela, mkoani hapa, amelazwa katika hospitali ya wilaya baada ya kumwagiwa mafuta ya taa na kuchomwa moto na mumewe ambaye ni mwalimu mstaafu, Boniface Mwakinyuke (64).

 
Kaimu Katibu Tarafa wa Ntebela, Cathbert Mwalukama alisema kuwa mwanamke huyo alimwagiwa mafuta ya taa mwili mzima kisha kuchomwa moto saa nne usiku hivi karibuni akiwa amelala fofofo.

 
“Siku hiyo walikuwa wote kwenye kilabu cha pombe lakini mke aliwahi kurudi nyumbani na alilala,” alisema Mwalikama.

 
Hata hivyo, baadhi ya watu waliokuwa kilabuni walioogopa kutaja majina walisema mwalimu huyo mstaafu alipoona mkewe kaondoka alianza ‘kulia’ wivu kwamba amechukuliwa na mwanaume mwingine.

 
Walisema mwalimu huyo baadaye alikwenda dukani na kununua mafuta ya taa lita moja na nusu na kiberiti na kwenda nayo nyumbani kwake ambapo aliyatumia kumlipua mkewe.

Baada ya kitendo hicho, wasamaria walimkimbiza mama huyo katika Kituo cha Afya cha Ipinda na baadaye akahamishiwa Hospitali ya Wilaya ya Kyela ambapo anaendelea na matibabu. Mwalimu huyo alikamatwa na kufikishwa Kituo cha Polisi Kyela ambako anashikiliwa.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Dk. Festo Ndungange amethibitisha kumpokea mgonjwa huyo na kusema amelazwa wadi namba tatu kwa matibabu zaidi.

Source:Global Publishers

Reactions:

0 comments:

Post a Comment