Baada ya kuvishwana pete ya uchumba, wasichana wengi huona kwamba kilichoko mbele yao ni kupanga harusi tu. Hujishughulisha kwa hali na mali kuhakikisha harusi inakuwa sawa na ile anayoiwaza siku zote, na kusahau kuwa baada ya harusi kuna maisha ambayo ndiyo haswa yanayopaswa kupangiliwa kwa umakini. Baadaye wanajikuta wameingia kwenye ndoa huku mambo mengi yakiwa hewani na hivyo kupelekea migogoro isiyoyalazima mara tu baada ya ndoa.
Kuna mambo muhimu sana ambayo wachumba wanapaswa wayaongelee na kufikia muafaka kabla ya kuunganika na kuwa mwili mmoja. Yanaonekana ya kawaida sana lakini yanaweza kuleta msuguano na kuharibu kabisa furaha ya ndoa. Tuyaangalie kwa uchache:
1. Mahali pa kuabudu.
Binti anaabudu katika kanisa kubwa na ndiye kiongozi wa sifa na muongozaji wa nyimbo karibia zote za kwaya, na kijana anaabudu kwenye kanisa dogo linaloanza na ndiye mwenyekiti wa vijana na mwalimu wa shule ya jumapili. Hapa nani anamfuata nani? Bila kukaa chini na kujadiliana kwa pamoja jambo hili linaweza kuleta mvutano. Ni vyema mkaangalia kwa mapana na marefu option zote kisha kwa pamoja mfikia muafaka kulingana na huduma ya kila mmoja wenu.
2. Jinsi ya Kuishi
Waafrika ni kawaida yetu kuishi pamoja na ndugu zetu na kusaidiana katika mambo mbalimbali ya maisha. Sio jambo geni kumkuta kijana au msichana anaishi na wadogo zake na kuwasomesha. Linapokuja suala la ndoa ni vyema jambo hili likawekwa sawa mapema. Je mtaweza kuishi na ndugu wangapi? Na wa upande upi na kwa kigezo gani? Je wataanza kuishi nanyi muda gani baada ya kuoana? Pale tu mtakapooana au lini? Hili si jambo dogo na linaweza kuharibu amani kabisa ndani ya nyumba. Ni vyema mkaliweka sawa mapema na wale mnaoishi nao wajue hawaishi tena na kaka au dada bali Mr & Mrs hivyo heshima iwe kwa wote. Pia sishauri kuishi nao mara tu baadavya kuoana, ni bora wakaenda kwa ndugu wengine angalau mwezi mmoja wa kwanza muweze kuwa na wakati wenu wa faragha wa kufahamiana vizuri na kuizoea nyumba yenu mkiwa wenyewe.
3. Mapato na Matumizi
Hili ni eneo nyeti sana. Wasichana wengine wanapoolewa huambiwa kuwa ‘usimwambie mumeo unapata kiasi gani na uwe na akaunti yako ya siri.’ Mmh hapa pana tatizo, maana nijuavyo mimi mwili mmoja ni katika kila idara, hamna siri. Sasa wewe ukificha na mwenzio akaficha, kuna maendeleo kweli hapo? Ni muhimu sana kwa wachumba kukaa na kupanga jinsi ya kuyatumia mapato yenu mtakapooana. Muwe wawazi kila mmoja anachokipata na muainishe matumizi yenu na kuangalia ni kwa jinsi gani mtaweza kuyafanikisha.
Baada ya kuoana, kila kitu kitakuwa ni chenu wote. Kama ulikuwa na nyumba, gari, viwanja, shares, bank accounts n.k vyote vinakuwa mali ya familia, hivyo ni vyema mkaangalia hili mapema ili asije mmoja wenu akajenga nyumba kwa siri bila mwenzie kujua. Pia muangalie ni ndugu gani wanahitaji msaada kifedha na jinsi gani mtaendelea kuwasaidia, mfano ada, matibabu, n.k. Hapa panahitaji hekima kubwa sanabya kiMungu kuamua nani asaidiwe kulingana na kipato chenu kwa wakati huo. Maana ndugu wa kuhitaji msaada wenu watakuwa ni wengi kuliko uwezo wenu. Hapa ndipo mstari wa mithali 14:1 unapoleta maana.
Mithali 14:1 Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.
4. Mipango ya Mbeleni
Shule, ujenzi, kuanzisha familia, kufungua biashara, kuanzisha huduma n.k yote haya yanahitaji kuzungumziwa mapema na kuwekewa misingi. Mfano wewe unahitaji baada tu ya ndoa utafute scholarship ukasome ulaya wakati mwenzio akifunga macho tu anajiona anaitwa baba, hapo lazima shida itatokea. Lazima mjue vipaumbele vyenu kama familia ni nini. Mkishafahamu hilo ni rahisi kujua muanzie wapi na wakati gani. Mume hawezi tu kuamka asubuhi na kusema anaacha kazi na kuanzisha kanisa, sasa familia itakula wapi? Ni lazima mkae chini mpange mjue mume akiacha kazi familia itaishije, mke je atakuwa tayari kubeba majukumu yote?
Mwisho huu ndio wakati muafaka kumweleza mwenzio kama uliwahi kuchumbiwa hadi kutolewa mahari lakini mambo yakaharibika. Pia kama unamtoto ni lazima narudia LAZIMA umweleze mwenzi wako. Usiingie kwenye ndoa na siri yoyote, itakuwa ni bomu la kuwasambaratisha.
Nakutakia ndoa njema yenye baraka, amani na furaha tele.
Source: Women of Christ
0 comments:
Post a Comment