Tuesday, August 28, 2012

Unafahamu hili..

Ndoto ya wasichana wengi ni siku moja kuja kuolewa. Mungu ametuahidi baraka zake nyingi ikiwamo baraka ya ndoa hivyo haupaswi kukaa na kusubiri hadi upate mchumba ndio uanze maandalizi yakupasa kuanza kujiandaa kuwa mke. Mungu amekuandalia mume mwema hivyo unapaswa kujiandaa mapema ili ndoa yako iwe bora.

1. Omba kwa ajili ya mume wako

Wasichana wengi wanaomba ili waweze kuolewa, hiyo ni sawa kabisa lakini jambo la kwanza kabisa inabidi uombe kwa ajili ya mume wako ambaye Mungu anaenda kukupatia. Anza mapema kuomba kwa ajili ya mume ambaye Mungu anaenda kukupatia. Omba kwa ajili ya maisha yake ya kiroho, uwezo wake kusimamia na kuitunza familia na maisha yake kwa ujumla. Usisubiri hadi uolewe ndipo uanze kuombea umoja katika ndoa yenu, anza sasa na pia kumbuka kuomba kwa ajili yako ili uwe mke mwema.

2. Jiandae

Familia yako unayoishi nayo ndio hasa sehemu yako ya kujiandaa kuishi na mume wako. Unapaswa kujifunza kuanzia sasa kuishi vizuri na watu wa familia yako, hutaweza kuishi vizuri na mume wako kama sasa unashindwa kuishi vizuri na ndugu na jamaa zako. Waonyeshe upendo, huruma na kujali na kwa kufanya hivi utakuwa umejijengea tabia ambayo utakuwa nayo kwa watu wote na mumeo pia. Unaposhindwa kukaa vizuri na watu wako wa karibu kama familia vivyo hivyo hautaweza kukaa vizuri na mume wako, ndoa haimbadilishi mtu bali inakuonyesha uhalisia wako. Jinsi ulivyo unapokuwa nyumbani kwenu ndivyo ulivyo.

3. Omba uweze kutambua hila za shetani

Sababu ya uhitaji wa kuolewa ulionao inaweza kuwa ngumu kugundua kama mtu anayetaka kukuoa hajatoka kwa Mungu. Sio kila nayesema Bwana asifiwe ni kweli ameokoka maana wengine wapo ili wapate wake wazuri, ndio maana ni muhimu sana kuomba uongozi wa Mungu ili uweze kujua nani hasa ametoka kwa Mungu. Pia inawezekana akawa ameokoka lakini akawa sio mume ambaye Mungu amekuandalia hivyo ni muhimu sana kuomba kwa ajili ya uongozi wa Mungu katika muda huu wa muhimu katika maisha yako.

4. Tulia mbele za Mungu

Filipi 4:6 Msifadhaike juu ya jambo lo lote; lakini katika kila jambo mjulisheni Mungu haja zenu, kwa kusali na kuomba pamoja na kushukuru

Mungu analifahamu hitaji lako na muhimu zaidi anakujua na kukupenda, hajakusahau maana hawezi kukusahau na anakuwazia yaliyo mema.

Ebrania 13:5b kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, “Sita kupungukia kamwe wala sitakuacha”

Yeremia 29:11 Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,’’ asema BWANA. “Ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru,ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo”.

Usikate tamaa, mume wako yupo na atakuja kwa wakati wa Bwana.

Endelea kumwamini Mungu. Ubarikiwe!




Source: Women of Christ

No comments:

Post a Comment