Thursday, August 9, 2012

Msaada Tutani...

Dada, nashukuru kwa muda wako unaojitolea kutuelimisha sisi na kwakweli kwangu binafsi umenifundisha mambo mengi na ninaendelea kujifunza mambo mengi pia kwa hilo nasema ahsante.

Dada mimi ni kijana niliyeoa na nina mtoto mmoja tatizo langu sio ndoa yangu tatizo langu ni ndugu zangu, nilivyokuwa nakuwa nilikuwa nalelewa na baba yangu mkubwa na mkewe kwani baba yangu alikufa nikiwa nipo darasa la tano ndipo wakanichukuwa na kukaa nami, mama yangu alikuwa anaishi mkoa mwengine na wala baba yangu mkubwa hakuniruhusu niende kwa mama yangu, na haikuwa ngumu kwangu kwani muda mwingi nilikuwa boarding shule nikirudi nyumbani muda unakuwa mdogo kwahiyo najikuta sing'ang'anii kwenda kwa mama.

Mama yangu kule alipo kumbe alishapata mume mwengine akazaa naye watoto wakike watatu hivyo ndiyo nilikuwa naambiwa na baba yangu mkubwa, ikafika kipindi mimi nilichotaka kuoa nikamwambia baba mkubwa na baba zangu wengine kwamba kwakuwa hawakuniruhusu niende kumuona mama basi. ningependa mama yangu awepo kwenye harusi yangu.

Baba zangu wakubwa na wadogo wakakaa kikao siku moja ilikuwa jumapili nakumbuka wakaniita na kunieleza mambo ambayo yamenichanganya mpaka leo, wakaniambia sababu ya kulelewa nao na sio mama yangu na sababu ambayo hawakutaka niende kwa mama yangu ni kwamba mama yangu mzazi alimuua baba yangu ndio maana wakanichukuwa na hawakutaka kitu chochote kutoka kwa yule mama kuja kwangu kwahiyo kwa vile sasa umeshakuwa na kukomaa huo ndio ukweli kwahiyo maamuzi yapo juu yako.

Kwakweli sitaficho nilichanganyikiwa sana, nilijiuliza maswali mengi ambayo nilishindwa kupata jibu nikaamua kwenda kumtafuta mama yangu labda yeye atanipa jibu, basi baba mkubwa akanielekeza mji aliokuwepo na majina yake yote akaniambia ukienda hospital ya mkuoa muulizie kwani yeye ni nesi pale, nami nikafanya hivyo nakuondoka kwenda kumtafuta mama.

Nilifanya kama nilivyoelekezwa lakini nilipofika hopsital wakaniambia mama yako ni mgonjwa sana amelazwa wakanipeleka mpaka kwenye wodi yani ni bahati tu nilienda maana kweli alikuwa anaumwa sana, aliponiona kabla sijajitambulisha akaniita "mwanangu" nilipatwa na uchungu wa ghafla na kujikuta nalia na yeye akaanza kulia na watu waliokuwepo wamekuja kumuona nao wakaanza kulia ikawa kama msiba sasa kila mtu analia, baadaye akaniambia hawa unaowaona hapa ni wadogo zako basi tukasalimiana na kuendelea kumuuguza mama.

Sikupata muda wa kuongea na mama nakutaka kujuwa ukweli kwakuwa mama alikuwa anaumwa sana na hakutakiwa kuongea muda mrefu alitakiwa kupumzika tu, huwezi amini siku ya nne baada ya mimi kwenda mama alifariki dunia!!!!! niliumia sana sio tu kumpoteza mama ambaye nilimuona na kumjuwa vizuri siku tatu tu bali alikufa bila mimi kujuwa ukweli kama alimuua baba yangu nakama ni kweli ni kwa sababu gani!!!!

Nikarudi kwa baba mkubwa nikamueleza yote wakasikitika kwamba sikuusikia ukweli ili niamini, ndoa yangu ikapngwa nikaoa na sasa nina watoto wawili, najuwa kwamba wale wodogo zangu baba yao pia aliumwa na kufariki dunia kwahiyo walibaki tu na mama yangu, roho inaniuma sijui niwasaidie ama hawanihusu kila mara nawafikiria ila sijui lakufanya nao, naombeni ushauri la kufanya maana baba zangu wakubwa wanasema hawataki kabisa kuwaona na hata wakija kukaa nyumbani kwangu baba zangu hawatakanyaga maana bado hawajamsamehe mama yangu, na upande mwengine nikiangalia baba zangu hawa ndio wamenilea mpaka nimefikia hapa kujitegemea leo niwaangushe?? kweli sijui la kufanya.

2 comments:

  1. Nyamizizi hii ni hadithi ya kweli au ya kutunga? Yaani mwanaume mzima anaamini upuuzi ambao upo tangu enzi na enzi ambao ni huu, mume akifa basi kauliwa na mkewe, tena hata kama huyo mume ndio kauleta ukimwi ndani akamuambukiza na mkewe, lakini akifa tu, mkewe mchawi kamuua.

    Ila ajabu akifa mwanamke, baada ya mwezi tu mume anaoa kimada/hawara yake maisha yanaendelea, hakuna cha kamuua mkewe wala mbona haombolezi msiba wa mkewe.

    Hayo hapo ndio mambo ambaya yanatokea sana kwenye jamii zetu, tukirudi kwenye kesi yako wewe kijana, peleleza mwenyewe ujue mirathi ya baba yako ilikuwaje hapo ndipo mara nyingi uchawi na ubaya wa mke unapoanzia!

    ReplyDelete
  2. Pole dada! Nadhani dini zote zinafundishwa KUSAMEHE, jaribu kukaa chini kuwaelewesha baba zako somo la kusamehe, ukizingatia ndugu yao amekufa na mama yako amekufa wasamehe na Mungu ndiye ajue siri zetu. Kuhusu wadogo zako hawana kosa lolote mimi navyoona so kama una uwezo please wasaidie kama kwako hawataki waje basi wapangie hata chumba, kama mama yako aliacha nyumba basi wasaidie wakiwa huko. Otherwise piga magoti mshirikishe Mungu atakujibu maombi yako. Ila please usiwaache wadogo zako.

    ReplyDelete