Tuesday, January 22, 2013

Shalom

Jambo hili limezua migongano mingi sana kwenye ndoa hadi kupelekea ndugu kuona kwamba mke au mume anamzuia ndugu yao kuwasaidia. Pia imeleta shida kwa wanandoa wenyewe kwa wenyewe. Tatizo maranyingi sio ndugu bali ni wanandoa, mmoja anapoamua kutoa msaada kwa ndugu wa upande wake bila kumshirikisha mwenzie.

Mume na mke ni mwili mmoja, haijalishi nani anakipato kikubwa, nani anafanya kazi au familia ipi inauhitaji mkubwa; haitakiwi na si sawa kwa mwanandoa mmoja kuwasaidia ndugu wa upande wake kimya kimya. Hili ni kosa ambalo limewagharimu wengi, mwenzio akigundua kuwa unasaidia ndugu zako hata kama ni kidogo kiasi gani bila kumshirikisha hatafurahia, ataumia kwa nini umemficha na atajiuliza ni mangapi mengine unamficha.

Usitoe chochote nje ya familia bila kumshirikisha mwenzi wako, kabla hujaamua kumsaidia mshirikishe mwenzi wako na kwa pamoja muamue msaada gani amtatoa na kwa kiwango gani na kwa muda gani. Pia kama mmeongea ikaonekana hamna uwezo wa kutoa msaada kwa wakati huo, usiende kusema mimi ningekusaidia lakini mwenzangu kakataa”,kwenye ndoa hakuna mimi na yeye bali wote ni mmoja hivyo mweleze hali hairuhusu kwa wakati huo.

Pia usimkaribishe ndugu kuja kuishi nanyi bila kuongea kwanza na mwenzi wako na mkakubaliana katika jambo hilo. Ni rahisi ndugu kusema nanyanyasika kumbe mwanandoa mmoja amechukua maamuzi ya peke yake na hivyo huyu aliyepuuzwa anamalizia machungu na hasira kwa ndugu aliyekuja. Matatizo mengi katika ndoa yatamalizwa kwa ushirikishwaji wa kina kwa wanandoa wote na kutokufanya jambo lolote bila kumshirikisha mwenzi wako.
 
Source: Women of Christ

0 comments:

Post a Comment