Tuesday, September 25, 2012

Uwezo wa Mwanamke...

 Wanawake tumepewa uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko pale tunapotambua nafasi tulionayo. Uwezo huu ni mkubwa zaidi kwa mwanamke anayemcha Mungu na mwenye nguvu ya Roho Mtakatifu. Tunaweza kubadilisha hali ya mahali ambapo watu hawana matumaini na wamekata tamaa na kuwafanya wapate tumaini kwa kuwapelekea neno la Mungu kivitendo kutumia uwezo wetu kama wanawake tukiongozwa na upendo wa Yesu.

Nimesoma kitabu kimoja kinaelezea jinsi ambavyo wanawake wanaomcha Mungu walisimama kidete na na kuleta tumaini, faraja, upendo na kuwaongoza watu kwa Yesu wakati wa uamsho katika miji mikubwa kwenye karne ya 19. Wanawake hawa walitumia uwezo wao kama wanawake kuwapa wahitaji chakula, wasio na makazi mahali pa kulala, kuwasaidia wazee na wasiojiweza, kuwapa neno la tumaini na msaada waliokuwa walevi kupindukia pamoja na wale wanaofanya biashara ya miili yao.
Waliwapa mahitaji ya miili yao huku wakiwafundisha neno la Mungu lenye uzima na injili ya msamaha ya Yesu Kristo. Walitoa mali, muda, elimu na nafasi zao kuwasaidia watu hawa. Waliacha na kujikana nafsi zao na kuwaangalia watu hawa ambao jamii ziliwatenga na kuwaona hawafai. Matokeo ya huduma hii miji mingi ilibadilika na watu wengi wakamrudia Mungu. Sio lazima uanzie mji mzima bali unaweza kuanzia pale ulipo.
Ni wangapi wanaishi maisha ya dhambi kupindukia ambao wapo karibu nawe? Wasaidie huduma za mwilini pale wanapohitaji katika upendo wa Kristo huku ukizungumza nao habari za Yesu na kwa kuuona ule upendo wengi watavutwa kwa Yesu. Watu wengi waliomezwa sana na dhambi hujiona kama hawastahili mbele za Mungu wala hawawezi kusamehewa, hivyo huzidi kudidimia zaidi na zaidi. Nyoosha mkono wako wa upendo ili uweze kuwarejesha kwa Yesu.
Yakobo 2:14-17 Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! ile imani yaweza kumuokoa? Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamuke yu uchi na kupungukiwa na riziki, na mtu wa kwenu akawaambia, Enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini?Vivyo hivyo na imani, isipokuwa na matendo, imekufa nasini mwake.

No comments:

Post a Comment