Wednesday, September 19, 2012

UUUiiiii watu wanasahau uchungu au ni nini...


Stori: Global Publishers

MWANAMKE mmoja ambaye jina lake halikufahamika mara moja, hivi karibuni alimtelekeza mwanaye wa kiume mwenye ulemavu wa viungo (pichani) katika duka la mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Michael Mwami, Mtaa wa Agrey, Kariakoo jijini Dar.
Tukio hilo lililoacha gumzo maeneo hayo lilitokea Agosti 19, mwaka huu ambapo mtoto huyo aliyekadiriwa kuwa na umri wa miaka mitano alitelekezwa na mama yake katika mazingira ya kutatanisha.
Akizungumza na Uwazi, Michael alisema: “Mwanamke huyo alifika hapa dukani kwangu saa 12:35 jioni na kuuliza bei ya bidhaa huku akiwa amembeba mtoto wake, baada ya muda akaniomba aniachie yule mtoto ili aende kujisaidia, aliacha na pochi lake pia hivyo nikaamini atarudi.
“Ulipita muda mrefu bila kumuona, mtoto akaanza kulia akimtaka mama yake lakini jitihada za kumpata hazikuzaa matunda. Tulifungua lile pochi ili kuangalia kuna nini, tukakutana na makaratasi kibao machafu, tukagundua kuwa yule mwanamke kamtelekeza mwanaye kiujanja,” alisema Michael na kuongeza:
“Nilichokifanya nilimbeba yule mtoto na kwenda kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha Msimbazi na kufungua jalada lenye namba MS\RB\5917\3012.”
Mtoto huyo kwa sasa yupo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jengo la watoto Makuti ‘B’. Afisa Ustawi wa hospitali hiyo, Nasensa Mjema alisema mwananchi yeyote anayemfahamu mama wa mtoto huyo atoe taarifa kwenye kituo chochote cha polisi kilichopo karibu naye.

No comments:

Post a Comment